Friday, May 30, 2008

SOMO LA LEO

ITAMBUE MILANGO YA KUTOKEA

UWAPO KATIKATI YA MAJARIBU NA HALI YA KUKATA TAMAA
Habari yako ndugu msomaji wa mafundisho haya, naamini ni kwa neema na huruma za Mungu kuwa leo tena tumepata nafasi ya kusogea mbele zake mungu ili tuweze kujifunza kitu kutoka kwake ambacho naamini kitakuwa na nafasi kubwa sana katika kubadilisha mifumo ya imani zetu na kujifunza kumuamini na kumtegemea Yesu peke yake bila kujalisha tunakutana na hali ya namna gani katika maisha yetu ya kila siku,
Kwako mpendwa msomaji
Majaribu na magumu tunayokutana nayo siku kwa siku si kwa ajili ya kutufadhaisha, kutuumiza, kutuvunja moyo, na hata kutuondoa kwenye mpango wa Mungu na hatimae kutupeleka jehanamu .Nivizuri ukaelewa hili siku zote kuwa, huo si mpango wa Mungu hata kidogo; lengo la Mungu, wakati mwingine anaporuhusu tujaribiwe ni kutaka kuimarisha imani zetu, kujitwalia utukufu, kujitukuza, kuwafanya wengine wamuamini na kumtegemea yeye tu kwa sababu ya muujiza uliofanyika kwako au utakao fanyika kwako maana upo muujiza utakaofanyika kwako mara baada ya kusoma mafundisho haya.

HIZI NI MOJA YA SABABU ZINAZOWEZA KUKUFANYA UPITIE KATIKA MAMBO MAGUMU

Ili ukue kiroho,Kiimani na uje kuwa msaada kwa wengine na hatimae kuyafikia yale Mungu aliyoyakusudia kwenye maisha yako, Ni vizuri ukafahamu kuwa kiwango chako cha kumuamini na kumtegemea Mungu kinategemea mambo yafuatayo, kama umemuona Mungu akikutetea katika madogo utamuamini katika hayo hayo madogo na utamtia moyo mtu mwingine katika hayo hayo madogo unayo yafahamu kuhusu Mungu na uweza wake.
Lakini kama Mungu amekuwa akionekana kwako katika makubwa na yaliyo onekana kuwa mazito kwako na yakukatisha tamaa kisha ukavuka salama, hutaacha kumuamini Mungu hata katika hilo lingine linaloonekana kuwa kubwa zaidi kwako, na kuwa na ujasiri wa kumtia moyo mwingine anaye pitia hayo, ndio sababu mtume Paulo alikuwa na ujasiri wa kumwambia Timotheo kuhusu magumu aliyokutana nayo na jinsi Mungu alivyo mtetea. Ukisoma 2Timoth 4:14-18 anaeleza, "Iskanda, mfua shaba,alionyesha ubaya mwingi kwangu;Bwana atamlipa sawasawa na matendo yake nawe ujihadhari na huyo, kwa sababu aliyapinga sana maneno yetu". Tunaona Paulo akiendelea kumueleza Timotheo kilicho tokea na hali ilivyokuwa na kitu anachotakiwa kujifunza katiaka hayo ukiendelea mstari wa 16 anaendelea "katika jawabu langu la kwanza hakuna mtu aliye simama upande wangu,bali wote waliniacha; naomba wasiesabiwe hatia kwa jambo hilo. Lakini Bwana alisimama pamoja nami akanitia nguvu,ili kwa kazi yangu ule ujumbe utangazwe kwa utimilifu,hata wasikie mataifa yote; nami nikaokolewa katika kinywa cha simba Bwana ataniokoa na kila neno baya,na kunihifadhi hata nifike ufalme wake wa mbinguni.utukufu una yeye milele na milele Amina" .Fikiria Kama Paulo asingekuwa ameyapitia hayo magumu, Kama angekuwa na kitu cha kumwambia Timotheo, anazungumzia habari ya Iskanda alivyoonyesha ubaya mwingi, anaendelea kumueleza jinsi alivyotegemea baadhi ya watu wangeweza kumtia moyo na kusimama pamoja nae na vile amabavyo hakuna mtu aliye simama upande wake. Kwa tafsiri nyingine inawezekana kabisa aliowategemea ndio waliomsaliti, tu kwa sababu ya kulisimamia kusudi la Mungu, na inafika mahari anaelezea kuwa aliokolewa na kinywa cha Simba ukiona anelezea haya yote uelewe wazi kuwa hayakuwa mapito ya kawaida, lakini pamoja na hayo tunaona Paulo akimtia moyo Timotheo kwa kumwambia kuwa pamoja na hayo yote Bwana alisimama pamoja nami akanitia Nguvu, akaniokoa na kinywa cha simba, ukiufuatilia ule mstari wa 18 anasema, "Bwana ataniokoa na kila neno baya." Kitu Paulo alichokuwa anasisitiza hapa kwa Timotheo ni kama Bwana alinipigania katika yote hayo hataacha kuniokoa na kila neno baya, hii inaonyesha alikuwa bado anaendelea na huduma na bado kulikuwa na magumu yanamkabili lakini alimtia Moyo Timotheo kuwa kama Mungu aliniwezesha huko nyuma hataacha kuniokoa na kila neno lililo baya. Leo hii wewe ni shahidi jinsi ambavyo watumishi Mbali mbali wamekuwa wakieleza jinsi walivyo pita katika magumu na hatimae Mungu akawasaidia. Kumbuka, kama wasingekuwa wamepitia hayo magumu, leo wasingalikuwa na kitu cha kukutia moyo na hata kukusaidia wewe kuvuka.
Wakati mwingine magumu hutokea ili kupanda Daraja kutoka imani uliyopo kwenda nyingine, kutoka utakatifu kwenda utakatifu na pia ili Mungu akuamini, Ni muhimu kufahamu kuwa hata wewe mwenyewe unapotaka kumuamini mtu ungependa kumpa mtihani japo tu kumpima uwezo wake, au kufanya jambo ambalo litapima endapo unachokiona kwake ndivyo kilivyo au ni cha kuigiza tu ili usije kumuamini kabisa na kumbe sivyo alivyo. Walimu wanaofundisha madarasani wanaelewa jinsi ambavyo kipimo cha kujua watu walielewa au la ni mtihani tu, na si vinginevyo, na mwanafunzi asiyetaka mtihani maana yake hataki Shule na hayuko tayari kwenda darasa lingine.Sasa ukisoma Yakobo 1:12 utakuta anasema "Heri mtu yule astahimilie majaribu; kwa sababu akisha kukubaliwa ataipokea taji ya uzima,Bwana aliyowaahidia wampendao."Nilipenda uone huu mstari unaosema akiisha kukubaliwa, hii ina maana kuwa ili Mungu akuinue, akuamini na akukubali unahitajika kushinda majaribu na sio kuishia tu kusema shetani alijiinua., Sasa ukisoma Warumi 5:3 utakuta anasema ,"wala si hivyo tu,ila na tufurahi katika dhiki pia;tukijua kuwa dhiki kazi yake ni kuleta saburi;na kazi ya saburi ni uthabiti wa moyo; na kazi ya uthabiti wa Moyo ni tumaini ,,,,,,,,,," ukiufuatilia huu mstari kwa makini utakuta unakutaka ufurahie jaribu,shida,au tabu yoyote unayokutana nayo, Nini sababu hasa? Sababu ni kuwa baada ya kushinda hilo jaribu, liko Tumaini, ipo faraja,na hatimae kukua kiroho, nakumbuka jinsi ambavyo tulipokuwa chuoni nikifanya masomo yangu ya awali, hakuna mtu alipenda kurudia mtihani{suplimentary} kama kuna kitu wanafunzi waliopo vyuoni huwa wanaomba usiku na mchana ni kutokuwa na sup maana wanaona inawapotezea muda lakini wale wanaorudia mtihani fulani wakisha kuufaulu vizuri huwa wanakuwa na uwezo mkubwa wa kumsaidia mwingine kwenye lile somo kuliko hata wale ambao hawakurudia mtihani. Hivyo unaweza ukapitia gumu fulani ili uwe na uwezo mkubwa wa kuwasaidia wengine.
Wakati mwingine majaribu huja, ili upate kuwa mkamilifu.
Ukisoma katika Yakobo 1:4 anasema "Saburi iwe na kazi kamilifu,mpate kuwa wakamilifu na watimilifu bila kupungukiwa na neno." Ni wazi kabisa kuwa baada ya kupita kwenye majaribu na mambo fulani yaliyoonekana kuwa magumu kabisa kwako halafu ukatoka salama, huwi tena kama ulivyokuwa hapo awali, maana ndani yako kunakuwa kumejengeka imani juu ya Mungu aliye kufanikisha, na walio wengi sana huanza kusimama kiroho baada ya kushinda vikwazo alivyokutana navyo. Mara nyingi imetokea watu wanapotoka kuokoka, wengine walipotengwa na marafiki,wazazi, kuchekwa ,kuchukiwa, kupewa majina Fulani Fulani ya dhihaka, hii ndio iliwasababisha kukaa kwenye maombi na kulisoma neno, na kwa sababu tu umeokoka kila unachofanya wanataka wachunguze kama ndivyo walokole huwa wanafanya au la,lakini ukifuatilia kwa umakini wengi hii ndio imewasaidia kusimama maana kila wakati wanajua kuna watu wanamtazama, hii inamsaidia kusimama kwenye maombi na kuwa mkamilifu mbele za Mungu, baadae nae anakuwa na ujasiri wa kumshauri mwingine. Nini kimemsaidia? Ni kuwa yale Magumu aliyokutana nayo awali yalisaidia kuujenga msingi wa utimilifu. Mtume Paulo alifika mahali akasema "nimevipiga vita vilivyo vizuri vya imani mwendo nimeumaliza imani nimeilinda." Ni kitu gani kilimpa ujasiri wa kusema amevipiga vita vilivyo vizuri vya imani na kwamba mwendo ameumaliza alafu imani ameilinda?Ujasiri huu ulikuwa ni kutokana na magumu mengi ambayo alikuwa amekutana nayo, na kuwa pamoja na hayo hakumuacha Yesu isipokuwa yakamfanya amtafute Mungu zaidi na kukaa zaidi katika hali ya kutaka kumuona Mungu akijidhihirisha kwake.Hivyo basi ni vizuri ukafahamu kuwa hatuwezi tukawa wakamilifu kama hatuta kabiliana wakati mwingine na vitu vya kutuvunja Moyo na vya kutukatisha tamaa kabisa kuna msemo mmoja husema kuwa"ili dhahabu ihakikiwe kuwa ni dhahabu safi hupitishwa kwenye Moto" kwa hiyo Moto ni kipimo cha kujua kama hiyo dhahabu ni ile safi au la. Ukisoma katika Isaya 43:1 anasema, "Lakini sasa, Bwana aliyekuhuluku,e Yakobo yeye aliyekuumba,e Israeli asema hivi, "Usiogope,maana nimekukomboa;nimekuita kwa jina lako wewe u wangu.".Sasa ukiufuatilia ule mstari wa pili utakuta anasema, "Upitapo katika maji mengi nitakuwa pamoja nawe na katika mito haitakugharikisha;uendapo katika moto hutateketea wala mwali wa moto hautakuunguza."Kitu ninachotaka ukione hapa ni hiki, Mungu anapoanza kujitambulisha kwako na kukuambia Usiogope maana nimekuita, tafsiri nyingine ya neno nimekuita inaweza ikawa nimekuchagua, sasa anapokuambia Usiogope maana yake ni kuwa anakutaadharisha, maana viko vitu utakutana navyo vitakuogopesha na anaposema upitapo katika maji mengi, maji mengi tunaweza tukayafananisha na misukosuko ya maisha. Mambo magumu kwenye maisha na vitu vya kukatisha tamaa .

japo pamoja na hayo alisha kuambia usiogope, na pia anaposema mito haitakugharikisha anamaana matatizo utayokumbana nayo hayata kufanya umuache Mungu kwa sababu yeye yu pamoja nawe,na anaposema uendapo katika moto hauta teketea ina maana kuna wakati utatakiwa kupita katika moto na mambo yatakayo kusababishia uchungu kabisa katika nafsi yako, lakini alisha kuambia kabisa, Usiogope maana yeye yu pamoja nawe katika vipindi vyote hivyo. Ndugu mpendwa unayefuatilia somo hili ni muhimu ukatambua kuwa mambo magumu ni sehemu katika maisha yetu Ili tukamilike, tuimarike na hatimae kukifikia kimo cha kristo.
Wakati mwingine magumu huja ili umtambue Mungu kwa sura nyingine, ambayo hujawahi kumuona akijidhihirisha kwako na hasa baada ya kufika mahali umekata tamaa kabisa.Sehemu nyingi Mungu alipotaka kujidhihirisha Kwa wale wasomaji wa Biblia watakubaliana nami kuwa kulitokea tatizo ambalo liliwafanya watu walie, wafikirie,wachanganyikiwe,watumie mda mwingi kuwaza tena bila kupata majibu, ukikumbuka habari za Esta baada ya chukuliwa mateka kutoka Yerusalemu wakiwa huko shushani ngomeni tena kama wakimbizi maana haikuwa nchi yao, Mungu anampa Esta kuwa malkia kwenye nchi ya watu akiwa yeye na kundi zima la Wayaudi walioingia huko kama mateka, baada ya kujisahau na kufurahi kuwa hata kama ni mateka bado wanaishi kwa amani kama vile wako kwao, na mtu wa kwao ndio amepewa umalkia, sasa wakiwa katika hali hii gafla inatokea kuwa wanatakiwa kuuwawa wayaudi wote mimi sijui kama kuna jaribu gumu kama lile la kutakiwa kuuwawa ukisoma Esta 3:8-11 anasema "Basi Haamani akamwambia mfalme Ahasuero, kuna taifa moja waliotawanyika na kukaa mahali mahali katikati ya mataifa walioko katika majimbo yote ya ufalme wako.na sheria zao zimefarakana na sheria za kila Taifa wala hawazishiki amri za mfalme ;kwa hiyo aimpasi mfalme kuchukuliana nao. Tunaona jinsi ambavyo Haamani haikumsumbua Esta kuwa malikia wa mfalme alichotaka hapa ni kutimiza hazma yake ya wayahudi kuuwawa tu, ukiendelea mbele kidogo inaonyesha wazi kuwa alikuwa ni Adui wa wayahudi hivyo akatengeneza maneno ya uchochezi ili tu wayaudi wauwawe, ukiendelea mstari wa tisa anasema basi mfalme akiona vema na iandikwe kwamba waangamizwe; nami nitalipa talanta kumi elfu za fedha mikononi mwao watakao simamia shughuli hiyo,waziweke katika hazina ya mfalme .ndipo mfalme alipoivua pete yake mkononi akampa hamani bin Hamedatha,mwagagi adui ya wayahudi. Kisha mfalme akamwambia hamani, hiyo fedha umepewa, na watu pia, fanya uonavyo vema. Sasa ukisoma ile sura ya 4 mstari wa 3 anasema "na katika kila jimbo ambako amri ya mfalme na mbiu yake imewasili palikuwako na msiba mkuu kwa wayahudi na kufunga na kulia na kuomboleza hata na wengi wakalala juu ya magunia na majivu" hii mistari inaonyesha walichanganyikiwa kabisa maana imeshatangazwa wanasubiri kifo na mfalme akisha pitisha amepitisha. Biblia inaposema "palikuwako na msiba mkuu", ujue haikuwa kilio cha kawaida wengine walijuta kuzaliwa,wengine lazima walitamka maneno magumu,maana hawakuona kingine isipokuwa mauti mbele yao, lakini hapa ndipo Mungu alipotaka kujidhihilisha kwao. Baadae ukiendelea kusoma utaona jinsi Mungu alivyowatendea miujiza wakaendelea kutawala na kumilki na hali waliingia kama mateka. Hivyo basi wakati mambo ya kukukatisha tamaa yanapo tokea na wakati mwingine utatuzi wa kibinadamu unapokataa ni vizuri ukamtumaini Mungu na kumfanya ajidhihirishe kwako. Yohana 14:21 anasema, "Yeye aliye na Amri zangu na kuzishika yeye ndie anipendae; nae anipendae atapendwa na baba yangu nami nitampenda na kujidhihirisha kwake." Ni muhimu kutambua kuwa Mungu amehaidi kujidhihrlisha kwako.Hivyo basi lolote unalo kutana nalo ni vizuri ukakaa mkao wa kuona Mungu akijidhihirisha kwako.USHUHUDABinti mmoja aliyemtumaini Mungu kuanzia utoto wake na kumuona Mungu akimfanikisha katika masomo yake kuanzia kidato cha kwanza mpaka alipokuwa akiingia kwenye mtihani wa kidato cha sita hakuna siku alitegemea yale yaliyotokea yangempata hakuamini kuwa kwa jinsi ambavyo Mungu amekuwa akimfanikisha kuna siku angekuja kukutana na mambo magumu namna hii, maana mpaka anafanya mtihani wa kidato cha sita hakukua na tatizo lolote, sasa baada ya matokeo kutoka ikaonekana hajapata daraja la kwanza la pili wala la tatu na la nne, kwa lugha ya leo ya wanafunzi wangesema alizungusha maana yake alipata sifuri, hakuna mtu aliamini au kuelewa kilichotokea,wazazi pia hawakuelewa , binti huyu alikuwa katika wakati mgumu sana hakuelewa kitu cha kufanya akaanza kuwa kama anaugua maono yake yalikuwa ni kuja kusomea Udaktari, sasa anaendelea vipi na amepata sifuri? Wakati mwingine inasemekana alikuwa anajikuta tu ana vidonge vingi mkononi na anasikia kabisa sauti ikimwambia "Si ujiue tu kuna haja gani ya wewe kuwepo Duniani, kwanza ndoto zako ndio zimekufa, hata mchumba gani atakaye kupenda wewe na hiyo sifuri yako?" Mara nyingi alisikia kukatishwa tama. Sasa mama mmoja aliyeokoka ambaye pia ni Muombaji, alikuwa ni ndugu yake huyu binti ndipo aliposikia hayo yaliyokuwa yakitokea akaenda kumchukua na kuishi naeAkaanza kumpa matumaini huku akimwambia Mungu anaweza, bado suala lako la kuwa Dactari lipo palepale njia za Mungu si njia zetu, Mungu atakufanikisha tu usiogope. Yule Mama aliendelea kumtia moyo huyu binti siku hadi siku, alipokuwa akiendelea kuishi nae akamshauri akachukue fomu za kurudia mitihani huku yeye akimlipia kila kitu na wakati huo akamtafutia mahali ambapo huyu binti alikuwa akifanya nursing kwa kipindi alichokuwa akisubiri kufanya mtihani.
Haikuwa jambo Rahisi kwa huyu binti maana hata wale wenzake aliokuwa akiwashinda Darasani walikuwa wamepata alama nzuri wengine wameshapata vyuo vizuri lakini yeye aliendelea kujitia moyo kwa Bwana na kuendelea kumtumaini Mungu peke yake. Baada ya mwaka kupita yule binti akawa amefanikiwa kufauru ile mitihani aliyo irudia kwa arama za juu sana na pale alipokuwa akifanya nursing palitokea watu kutoka nje ya nchi ambao walikuwa wanahitaji watu wakawasomeshe udaktari Nchi za ulaya kutoka kwa wale manesi ambao na yeye ni mmoja wao walipohitajika watu watatu yeye alipita bila kipingamizi maana kwanza alikuwa amefauru vizuri ile mitihani aliyokuwa ameirudia na akawa anaelimu nzuri kwa pale, baadae akaenda kusomea udaktari tena nchi za Ulaya aliporudi akawa ni moja ya madaktari wachache wanaoaminika hapa Nchini. Hivyo basi Mungu anapokuwa ameruhusu jambo fulani litokee huwa anataka kujitukuza ni wazi kabisa kuwa huyu Dada inawezekana alipenda kusomea udaktari lakini hakutegemea ingekuwa ni Ulaya, ninachotaka ujue ni kuwa muujiza wako upo, usijali ni hali ya namna gani unayopitia Muamini Mungu.
Mtume Paulo alipokuja kugundua kuwa magumu aliyokuwa akipitia ni kwa ajili ya udhihirisho wa nguvu za Mungu kwenye maisha yake alifika mahali akafurahi hata alipopita kwenye matatizo ukisoma 2korinto 12:9 anasema "Nae akaniambia,Neema yangu yakutosha;basi nitajisifia udhaifu wangu kwa furaha nyingi,ili uweza wa kristo ukae juu yangu.kwa hiyo napendezwa na udhaifu,na ufidhuli,na msiba,na adha,na shida,kwa ajili ya kristo.maana niwapo dhaifu ndipo nilipo na nguvu." Sasa kwanini mtume Paulo akasema niwapo dhaifu ndipo nilipo na nguvu maana yake ni hii, kila udhaifu uliokuwa ukija kwenye maisha yake ulikuwa na nafasi ya kumfanya aone nguvu za Mungu kwa namna ya tofauti,au aone miujiza totauti, au amtambue Mungu kwa sura tofauti. kila Mungu alipomsaidia katika mambo ya kukatisha tamaa aliyokutana nayo alipata nguvu kubwa ya kusonga mbele na kutojali magumu ambayo yamkini yangekuwa mbele yake, ndipo sasa akatambua na kusema "niwapo dhaifu ndipo nilipo na nguvu." Mungu alivyo jidhihirisha kwa Paulo
Saa hii Paulo na Sila wakiwa wamekamatwa na kupigwa sana kisha kufungwa kwa mikatale na wamewekwa gerezani hakuna mtu angeweza kukubaliana nami kwa kipindi kile kuwa Mungu aliruhusu yale yatokee kwaajili ya utukufu wake, yaani kwa ajili ya kujidhihirisha, maana kwa wasomaji wa Biblia ni lazima wataungana nami kuwa haikuwa mara ya kwanza kwa Paulo kuwekwa gerezani na Biblia inasema wazi kabisa kuwa kwa safari hii walikuwa wamepigwa sana na pia walikuwa wamefungwa kwa mikatale na si hivyo tu hebu soma hii uone Mat 16:22 anasema, "makutano yote wakaondoka wakawaendea makadhi wakawavua nguo zao kwa nguvu wakatoa amri wapigwe kwa bakora."Sasa sio rahisi sana kuelewa kuwa pamoja na hayo yote bado Mungu alikuwa pamoja nao inawezekana kabisa ungekuwa wewe au mimi tungesema kama ni kazi ya Mungu basi iache maana ni rahisi kufanyiwa mambo mengine na si kutolewa Nguo hadharani,yaani jana umemuongoza mtu sala ya toba hapo na una watoto wa kiroho, leo wanaona ukidhalilishwa tena kwa kutolewa nguo na kuchapwa bakora inaweza isiingie sana akilini ni ngumu kuelewa, mstari wa 23 anasema na "Walipokwisha kuwapiga mapigo mengi,wakawatupa gerezani,wakaamuru walinzi wa gereza wawalinde sana nae akisha kupata amri hii akawatupa katika chumba cha ndani,akawafunga miguu kwa mikatale.’Sasa kwa nini nasema muda wote huu Mungu alikuwa pamoja nao na aliacha tu yote hayo yatokee ili ajidhihilishe kwao na kwa wale waliowakamata. Ukisoma mstari wa 25 anasema "Lakini panapo usiku wa manane Paulo na sila walikuwa wakimuomba Mungu na kumuimbia nyimbo za kumsifu na wafungwa wengine walikuwa wakiwasikiliza." Sijui kama unaona kama mimi ninavyoona kwamba kama wafungwa wengine walikuwa wakiwasikiliza inamaana Mungu alitaka hata hawa wafungwa waipate ile injili, Na je wangeipataje kama Paulo na Sila wasingekaa nao mle gerezani na wangekaeje gerezani kama yaliyotukia hayakutukia? Sasa ukiangalia ule mstari wa 26 anasema "Ghafla pakawa tetemeko kuu la nchi" kumbuka ni baada ya Paulo na Sila kumuomba Mungu na kumuimbia nyimbo za sifa na baada ya wafungwa wengine kuipata injili yao endelea"hata misingi ya gereza ikatikisika,na mara hiyo milango ikafunguka,vifungo vya wote vikalegezwa,"Hebu nikuulize swali, inamaana walipokuwa wakipita katika misukosuko Mungu alikuwa haoni na unafikiri hawakuomba wakiwa wanapigwa bakora? Sasa kwa nini Mungu alinyamaza halafu anakuja kufanya miujiza mikubwa huku mbele ya safari? Hii ni lazima Mungu alitaka kujidhihiriisha kwa nanmna ya tofauti, tena si kwao tu, isipokuwa na kwa maaskari na wafungwa wengine. Hebu tuendelee mstari wa 27 anasema "Yule mlinzi wa gereza akaamka,nae alipoona yakuwa milango ya gereza imefunguka,alitafuta upanga,akataka kujiua akidhani ya kuwa wafungwa wamekimbia ila Paulo akapaza sauti yake akasema, usijidhuru,kwa maana sisi sote tupo hapa." Sasa kwa nini nilisema Mungu alikuwa na kusudi pia maaskari na wafungwa wapate injili ili pia waokoke. Mstari wa 26 anasema "akataka taa ziletwe yule polisi sasa akirukia ndani, akitetemeka kwa hofu,akawaangukia Paulo Sila, kisha akawaleta nje akasema Bwana zangu,yanipasa nifanye nini nipate kuokoka?wakamwambia mwamini Bwana Yesu nawe utaokoka pamoja na nyumba yako." Sasa ukiendelea kusoma yaliyotokea hapo mbele utaona jinsi ambavyo usiku uleule Yule mlinzi wa gereza akawapeleka nyumbani kwake Paulo na sila, na Biblia inasema watu wote wa nyumbani mwake yule Askari waliokoka na yeye mwenyewe Askari ndie akawahudumia kuwaosha mapigo yao akina Paulo na nyumba nzima wakabatizwa siku hiyo hiyo na Biblia inasema akawaandalia chakula. Sasa sitaki kuelezea zaidi kilichoendelea kutokea isipokuwa Mungu alifanya maajabu na ishara nyingi sana kwa Paulo na Sila baada ya tukio hili.
Kitu ambacho ninatamani ukifahamu ni hiki, kuwa wakati mwingine unapokabiliana na magumu tena ambayo hujawahi kuyategemea kabisa sio rahisi kufikiri kuwa eti Mungu anaweza akawa anataka ajidhihirishe katika hilo na kuwa bado Mungu yupo pamoja nawe. Wengi huona Mungu yupo mbali kabisa na amewaacha lakini Mungu anasema katika Yeremia 23:23, "Mimi ni Mungu aliye karibu mimi si Mungu aliye mbali." Na wengine huanza kutafuta ni wapi wamekosea, hii ni nzuri lakini wakati mwingine Mungu huwa anaruhusu kwa ajili ya kusudi lake alilonalo kwako mbele ya safari, na hasa katika kukudhihirishia wewe na wengine uweza wake.Mungu alitaka kujidhihirisha kwa wana wa Izraeli
Ni rahisi sana kufikiri kuwa Mungu alikuwa hajui kuwa Mbele yao kuna Bahari ya shamu, wakaendelea tu kwenda pia kumbuka yeye ndie alikuwa anawaongoza lakini utajiuliza kwa nini Bado aliwaacha waende kwenye bahari ya shamu lengo lake lilikuwa ni kwenda kujidhihirisha kwao na wengi wetu tunafahamu kabisa kuwa Mungu alikwenda na kuigawanya bahari, kitu ambacho hakuna mtu mwenye akili za kibinadamu angefikiri kingeweza kutokea lakini baada ya kutendewa muujiza huu walimuamini Mungu kwa kiwango cha juu sana na kuwa na hakika kuwa hakuna lisilowezekana kwake, hivyo basi wakati mwingine Mungu huwa anataka ufike mahali pa kumuamini kwa kiwango cha tofauti ili usimuonee mashaka tena.
Wakati mwingine magumu hutokea ili ufike mahali Mungu alikotaka ufike .Si wengi sana huwa wanaamini kuwa wakati mwingine Mungu huwa anaruhusu jambo fulani litokee ili yeye afike pale Mungu alipomkusudia, ni wazi kabisa kuwa unaweza kukutana na kashikashi nyingi sana za kimaisha na mambo ya kukuvunja Moyo lakini ikawa ndio njia yako ya kuyaendea mafanikio yako, wakati mwingine inaweza ikawa ni kwa maumivu na machozi lakini ikawa ndio muujiza wako.Ukifuatilia vizuri kwenye Biblia utamkuta kijana Yusufu ambaye Mungu alimkusudia kwenda kuwa mtawala kule Misri ili afike Misri na kuwa waziri mkuu kama Bwana alivyomkusudia ilimbidi kwanza achukiwe na ndugu zake,maana kama wasingelimchukia wasingelimtupa shimoni na baadae kumuuza, maana kule kumuuza ndiko kulikokuwa kunalitimiza kusudi la Mungu kwa ajili ya yeye kwenda Misri, japo yeye pamoja na nduguze wote walikuwa hawajui kitu ambacho Mungu alikuwa anafanya. Ukisoma Mwanzo 39 mstari wa kwanza anaanza kukuonyesha maisha ya Yusufu baada ya kufika Misri kama mtumwa.Ukifuatilia kwa namna ya kawaida inawezekana lazima Yusufu alilia sana,aliumia, na pia kujeruhika kwa kuwa nduguzake walimchukia kiasi cha kumuuza, lakini kama hayo yasingelitokea kusudi la Mungu lisingelitimia,
Na pia tunaona wazi kuwa alipofika Misri si kuwa mambo yake ndio yalikuwa shwari moja kwa moja, isipokuwa ndio akasingiziwa kuwa alitaka kubaka na kutiwa gerezani sasa kwa wale wanaofuatilia Biblia watagundua wazi kuwa ulikuwa ni mpango wa Mungu kwa Yusufu kwenda gerezani ili atokee gerezani kwenda kwa mfalme{ikulu} na ndipo litimie lile Mungu alilolikusudia kwa yeye kuwa waziri mkuu, hili ni jambo la kukutia moyo sana maana inawezekana kabisa unapitia mambo magumu kumbuka utakaposhinda ndipo utakapogundua kuwa Mungu alikuwa na makusudi kwa wewe kuyapitia hayo. Ili kufika pale alipopakusudia kwa ajili ya maisha yako.
Nakumbuka jinsi ambavyo kaka mmoja alinipa ushuhuda baada ya kusoma moja ya vitabu nilivyo andika na hiki kilikuwa na kichwa SABABU 12 ZA WATU KUKATA TAMAA, KUJERUHIKA, KUVUNJIKA MOYO, NA KUPOTEZA MATUMAINI.Alisema nilikuwa nimemuomba Mungu kwa ajili ya kwenda chuo na hatimae nikapata chuo kilichoko Dar es salaamu,lakini Ada yake ilikuwa ni kubwa maana nilitakiwa kujilipia mwenyewe, nikaendelea kujiandaa kuelekea huko, huku nikiendelea kumuomba Mungu anisaidie kujua kama hapo ndipo mahali hasa nilipotakiwa kwenda, na siku ya kuripoti ilipofika nilikuwa tayari nina pesa taslim zaidi ya laki tatu mkononi kwa ajili tu ya kuripoti, anasema nilipofika Dar tayari kwa kuripoti mara nikaibiwa pesa yote na matumaini yangu ya kusoma yakaishia pale, maana sikujua nitapata wapi pesa nyingine na mda ndio unapita siwezi tena kuja kwenye hicho chuo,ikanibidi nirudi kwetu Dodoma nikiwa na uchungu mwingi Rohoni kwa sababu nimeibiwa pesa ambayo ndio niliitegemea, na chuo pia nikawa nimekikosa.Anasema alikuwa katika hali mbaya sana akiwa katika hali hiyo akaendelea kumuomba Mungu pasipo kukata tamaa, ndipo baada ya miezi kadhaa kupita akapata nafasi ya kwenda kwenye mkoa Fulani ambako alienda tu kutembea na kupumzika baada ya yaliyomkuta kutokea anasema nikakuta chuo wanachofundisha mambo ambayo hasa ndio niliyokuwa nikiyataka na Ada yake ni kama Robo ya ile niliyotakiwa kulipa kule Dar es salaam pia nikawakuta watu niliowahi kusoma nao kwenye chuo changu cha awali,anasema nilifurahi sana kwani nikaona pale hasa ndipo Mungu aliponikusudia yaani ninaamani na ninaziona ndoto zangu zikitimia.Ushuhuda huu ni kwa ajili ya kutusaidia kujua kuwa wakati mwingine mambo yako yanaweza yakakwama tu kwa sababu njia uliyoipitia sio uliyotakiwa kuipita au njia unayotaka kupita si sahihi sasa ili urudi kwenye mstari huwa ni lazima ulipe gharama.
Na mfano mwingine ni huu, kuwa vijana wengi leo wanao chumbia au kuchumbiwa na watu ambao sio wale Mungu alio wakusudia kwenye maisha yao. Huwa wanapata shida sana Mungu anapokuwa kazini kuwatoa huko ambako sio sahihi wao kuwa au kuelekea , kumbuka neno lake limehaidi utafundishwa na utaongozwa mahali ambaoko ni sahihi Zab 32:8 Nitakufundisha na kukuonyesha njia utakayoiendea;nitakushauri,jicho langu likikutazama" Maana kama Mungu ameona unaelekea kwenye,majuto, kukosa amani,kwenye vilio, kwenye kuacha wokovu, au kufa kwa huduma yako mara nyingi huwa anaruhusu mazingira ya kukukatisha tamaa kabisa juu ya mpango huo,ili baada ya hapo akupitishe kwenye mpango wake ulio sahihi, sasa kwako inaweza ikaja kama mapito au jaribu jitie Moyo kwa Bwana ukiamini kuwa Mungu anao mpango kamili juu ya maisha yako.Maana kama unamtegemea Mungu huwa hawezi akaruhusu mabaya yatokee kwenye maisha yako, sasa mfano huyu Dada hakutakiwa kuwa na huyu kaka aliyenae anaweza tu kushitukia ameachwa , au Mungu anaweza akatumia watu kukushauri, maana neno lake limesema atakushauri, pia jambo lolote laweza kutokea tu mradi msiwe pamoja, nirahisi sana kuumia maana tayari ulikuwa umempa nafasi ndani ya moyo wako,kulia,kujeruhika, hata kuona una bahati mbaya, na kuona Mungu amekuacha na hali Mungu anasema sitakuacha wala sitakupungukia ni wachache sana ambao huwa wanaangalia na upande ule wa pili kuwa inawezekana Mungu ameniepusha na jambo baya au inawezekana huyu hakutakiwa kuwa nami kwenye maisha, wengi huwa wakuja kuelewa baadae sana baada ya kukutana na mtu amabae Mungu alikuwa hasa ndio amemkusudia kwenye maisha yake, mtu atakae inua huduma yake,atakae saidia familia yake, na atakae mfanya aishi maisha ya amani na furaha.
Wakati mwingine majaribu ni kwa ajili ya kuufanya uhusiano wako na Mungu uendelee kukua siku hadi siku au ubadilike kabisa. Ni muhimu sana ndugu msomaji ukafahamu hili, kuwa kila unaposhinda vikwazo na majaribu uhusiano wako na Mungu huwa unakuwa, maana Mungu anaporuhusu jaribu kwako huwa kunakitu anataka kuona kwenye maisha yako na wakati mwingine si tu kuwa Mungu anaruhusu majaribu na kuyazuia isipokuwa kuna wakati yeye mwenyewe anaweza akakujaribu ukisoma Mwanzo 22:1 anasema "Ikawa baada ya mambo hayo Mungu alimjaribu Ibrahimu,,,,,,,,,"nilichotaka hapa uone ni kuwa Mungu alimjaribu Ibrahimu na wala si shetani, hivyo basi si kila jaribu ni shetani, Mungu alimjaribu Ibrahim kwa kumtaka amtoe Isaka, kumbuka halikuwa ni jaribu la kawaida kama unavyoweza kufikiri kwa haraka haraka, uelewe wazi Isaka ndie aliyetakiwa kuwa mrithi, na wakati huo Ismaili alikuwa amesha ondoka, na Ibrahimu amehaidiwa uzao kama nyota za Mbinguni hakikuwa kitu cha kueleweka kabisa maana huo uzao unatokea wapi ikiwa Isaka anakufa, sasa ukisoma ule mstari wa 15 unasema, "malaika wa Bwana akamwita Ibrahimu mara ya pili kutoka mbinguni akasema nimeapa kwa nafsi yangu asema Bwana kwa kuwa umetenda neno hili wala ukunizuilia mwanao,mwanao wa pekee,katika kubariki nitakubariki na katika kuzidisha nitakuzidisha uzao wako kama nyota za mbinguni na kama mchanga uliopo pwani;na uzao wako utamiliki mlango wa adui zao ukiusoma ule mstari wa 18 anasema na katika uzao wako maaifa yote a dunia watajibarikia; kwa kuwa umeitii sauti yangu" kitu nilitaka uone ni kuwa, uhusiano wa Mungu na Ibrahimu ulibadilika kabisa baada ya kukubali kwenda kumtoa Isaka, kwa tafsiri nyingine baada ya kulishinda jaribu maana Mungu alikuwa anasubiri aone kama atashinda au la na ndio maana mwishoni akamaliza kwa kusema, kwa kuwa umeitii sauti yangu tungeweza kutafsiri kama kwa kuwa umelishinda jaribu. Akisema kwa kuwa umeitii sauti yangu maana yake ni kuwa kama usinge itii au kama usinge lishinda jaribu haya ninayo kubarikia na kukuahidi yasingelitokea kwako,
Ndio sababu ni muhimu kujitahidi kuhakikisha unashinda Majaribu au mapito unayokutana nayo maana saa hii, huwezi kujua kuna muujiza gani utatokea mara baada ya wewe kulishinda hilo jaribu, ukisoma katika "Ufunuo 2:17 anasema Yeye aliye na sikio, na alisikie neno hili ambalo Roho ayaambia makanisa: Yeye ashindae nitampa baadhi ya ile mana iliyofichwa,nami nitampa jiwe jeupe, na juu ya jiwe hilo limeandikwa jina jipya asilolijua mtu ila yeye anayelipokea" anasema yeye ashindae nitampa, hii inamaana kuwa si kila mtu isipokuwa ni yeye ashindae tu, sasa ukifuatilia pale chini anasema nitampa jiwe jeupe na juu ya jiwe hilo limeandikwa jina jipya,maana yake ni hii utakaposhinda tegemea jambo jipya kwenye maisha yako.
Wakati mwingine lile unaloliona jaribu linaweza kuwa ni mpango wa Mungu katika kukuepusha na hatari Fulani,Mfano huu utakusaidia, Kaka mmoja aliachwa na mke wake tena kwa hila kabisa, na yule Dada akasema hamtaki na hampendi kabisa yule kaka. Wanandugu wakajaribu kuingilia kati ikashindikana kabisa yule Dada aligoma kabisa kurudiana na huyu kaka na hali alikuwa ni mume wake, kitu kilichofanya watu waanze kutafuta kujua ni kosa gani kubwa hasa alilolifanya huyu kaka, lakini wakimuuliza huyu kaka anasema anashangaa hata yeye aelewi na walikuwa wamezaa watoto wawili tu, siku moja huyu Dada akamwambia rafiki yake wa karibu sana{kwa tafsiri ya leo tunaweza sema msiri wake} akasema hivi si kwamba simpendi Mme wangu isipokuwa nilitembea nje ya ndoa, Mume wangu alipokuwa masomoni hivyo nimeathirika na sipo tayari yeye ajue na wala sitaki kumuambukiza ukimwi,maana ni nani atalea watoto wangu nikifa na endapo na yeye atakuwa ambukizwa, niliposikia ushuhuda huu nilishangaa sana. Sasa kwa upande wa huyu kaka inakuwa ni huzuni na kuona ameachwa pia kuona Mungu hamuoni kuona amedharaulika kumbe Mungu aonae sirini anamuepusha na Hatari ya kuambukizwa virusi viliyokuwa vinakuja mbele yake, japo haina maana kila anayepitia haya iko namna hii, kwanza Biblia imekataa kuachana, nilitaka tu ujue kuwa wakati mwingine Mungu anakuwa anakuepusha na jambo Fulani baya zaidi, mara nyingi inakuwa si rahisi kwa wakati huu kuelewa ila ukimtumaini Bwana kwa Moyo wako wote hata hali ingeonekana kuwa mbaya kwa kiwango gani Biblia imesema tumaini la mwenye haki halitabatilika. Pia ukisoma Isaya 60:2 anasema "Maana tazama giza litaifunika dunia, na giza kuu litazifunika kabila za watu; bali Bwana atakuzukia wewe na utukufu wake utaonekana juu yako." Hivyo basi inawezekana kabisa mambo yote yakaonekana kuwa ni giza tupu kwako maana mambo unayokutana nayo hujawahi kuyategemea, kumbuka utukufu wa Bwana utaenda kuonekana juu yako endapo utaendelea kumtegemea na kumuamini hata katika hali hiyo unayokutana nayo sasa.
Nimekuwa nikijiuliza maswali mengi sana huku nikindelea kumuomba Mungu baada ya kufanya ushauri na baadhi ya watu ambao wao waliniambia walimuacha Yesu kwa sababu walikutana na majaribu mazito,na wengine wameacha huduma walizokuwa wakifanya kwa sababu ya majaribu na magumu wanayopitia wengine waliniambia wameanguka kwenye uzinzi baada ya majaribu makali, wengine hunijulisha jinsi ambavyo wapo katika hali ya kukata tamaa hivyo wanahitaji maombi ndipo Mungu alipoendelea kunifundisha hili somo.
Hii ni moja ya mifano ya watu wanao pita kwenye majaribu na hali za kukatisha tamaa
Wapo wanawake ambao walipokuwa wanajifungua kwa mara ya kwanza watoto walikufa na kwa sababu ya matatizo yaliyotokea wakafungiwa uzazi,maana yake hawawezi kuzaa tena, sasa ebu fikria jinsi ambavyo tayari yeye na mume wake walikuwa na matumaini na mipango mingi juu ya watoto wao ambao Bwana angewapa gafla unaambiwa mtoto amekufa na kizazi kimefungwa,hili si jambo rahisi hata kidogo, nakumbuka Dada mmoja alinijulisha jinsi ambavyo alipata BP akiwa ni mjazito na baadae mtoto akafa tumboni akafungiwa uzazi.Anasema alichanganyikiwa,na anatamani sana kuzaa lakini aliambiwa na Daktari kuwa akizaa tena atakufa .Kumbuka "yaliyoshindikana kwa mwanadamu kwa Mungu yanawezekana." ushuhuda huu utakusaidia nilikuwa naongea na rafiki yangu ambae ni Daktari aliniambia jinsi ambavyo inakuwa haiwezekani kabisa wao kuamini kuwa baada ya kumfunga mtu kizazi anaweza akajifungua tena sasa anasema siku moja alishangaa kuona mama aliyemfunga tumbo la uzazi ni mjamzito na kuwa aliombewa, anasema wakati wa kujifungua walimfanyia operation na kukuta mtoto amekaa nje ya utaratibu wa kibaolojia nina maana nje ya tumbo la uzazi ila amejishikiza mahali ambapo anapata mahitaji yote muhimu kutoka kwa mama, alivyosema yeye ni kuwa kuanzia hapo alianza kuamini kuwa Mungu anaweza kufanya maajabu na alinielekeza kuwa zamani alikuwa hawezi kabisa kuamini kitu kama hicho kwa jinsi walivyo somea hayo mambo, kumbuka Yeremia 32:27 inasema "Tazama,mimi ni Bwana,Mungu wa wote wenye mwili;je kuna neno gumu lolote nisiloliweza?" Anaposema yeye ni Mungu wa wote wenye mwili maana yake ni kuwa yuko juu ya wote wenye mwili,wasomi, wanasayansi na madaktari na watu wanaofanya mambo makubwa leo Duniani,wote hawa ni kuwa wanakijisehemu tu cha maharifa aliyowapa, hebu jiulize hili swali kama Yesu alizaliwa kama mwanadamu si angetakiwa kufuata taratibu zote za kibinadamu lakini Biblia inasema mimba ilikuwa ni kwa uweza wa roho mtakatifu maana yake ni kuwa utaratibu wa kisayansi na kibaiologia haukufuatwa lakini hii haikusababisha yeye asizaliwe kwa sababu Mungu ni mungu wa wote wenye mwili na njia zake si njia zetu, watumishi wakilitambua hili hawataona shida kuwaombea watu wenye kansa, wenye ukimwi na matatizo ya uzazi, kwa sababu aponyae si wao ila ni Mungu ambae hakuna neno gumu kwake lisilowezekana, pia wanaomuamini Mungu wakilitambua hili hawataacha kuendelea kumuamini na kumtegemea yeye peke yake.na kukaa mkao wa kusubiria miujiza yao.
Wapo watu ambao walitegemea mambo makubwa sana kabla ya kuolewa au kuoa hawakuwahi kufikiri habari za mapito ya ndoa na magumu ambayo wangeweza kukutana nayo, wengine wao kwa sasa wanatamani kama ingetokea nafasi ya kuoa au kuolewa tena, hii yote ni kutokana na magumu wanayo kutana nayo, nakumbuka Mama mmoja alipokuwa akitushirikisha kwa habari za kumuinua kwenye maombi alitujulisha jinsi ambavyo Mume wake ambae hajaokoka alimvizia kumuua kila siku, na kuwa kila alipotaka kufanya hivyo alimuona., sasa Mume wake amekuwa akishindwa kutimiza azma iyo kwa muda mrefu na hali hii imemfanya huyu mama kuishi kwa mashaka makubwa sana, pia wapo wanawake walio olewa na wanaume wasiomjua Mungu kumbuka huyo ni mme wako na umeshafunga nae pingu za maisha ni kifo tu ndicho kitakachowatenganisha hata kama anakukera vipi, usikate tamaa endelea tu kumuamini Mungu kwa ajili yake. Elewa kuwa njia za Mungu si njia zetu mawazo ya Mungu si mawazo yetu ipo siku Mungu atakutana nae inawezekana unapata tabu na huyo mke, Elewa tu kuwa Mungu ajashindwa, wapo watu wengine inafika mahali anakuambia ameomba mpaka sasa amechoka ni muhimu ukatambua kuwa hakuna haja ya kuchoka, muujiza wako uko njiani unakuja hebu tuone Biblia inasema nini juu ya hilo "Luka 18:1 Akawaambia mfano ya kwamba imewapasa kumuomba Mungu siku zote wala msikate tamaa" Sasa ukifuatilia huu mstari kwenye tafsiri zingine za kiingereza utakuta lile neno {siku zote} limeandikwa {always} maana yake kila wakati hivyo basi muombe Mungu kila wakati juu ya hilo jambo linalokukera maana ujui ni wapi na sa ngapi Mungu atatenda muujiza wako.Nakumbuka tulienda kufanya huduma mkoa fulani, hivi karibuni sasa tulikuwa na mwenzetu mmoja ambae ana kaka yake na familia wamekuwa wakimuombea sana amjue Mungu hakikutokea kitu mpaka wakafika mahari wakasahau kwa Kiswahili kingine wakachoka au wakamuachia Mungu kama wengi leo wanavyopenda kusema, wakifika mahali wamekata tamaa, sasa tukiwa kwenye huo mkoa yule kaka yake alihudhuria kipindi cha usiku ambacho tulikuwa tukiwafundisha watu waliokoka namna ya kusimama kwenye wokovu, tena nakumbuka tuliwafundisha kwa njia ya kuonyesha mkanda wa video na ukumbuke yule kaka alikuja tu kwa sababu ndugu yake alikuwepo hivyo alikuja kama kumsalimia kwa sababu alijua yupo pale kwenye lile eneo la huduma, kilichotokea ni kuwa ikabidi ajumuike na wengine kuangalia ile filamu maana tulikuwa kwenye huduma, sasa ilipofika saa ya watu ambao hawajaokoka kumpa Yesu maisha wakashangaa kuona yule kaka akinyosha mkono na kumpokea Yesu, yule ndugu yake hakuamini kilichotokea ilibidi atoe ushuhuda kuwa walikatatamaa, hakuna mtu alitegemea angeokoka tena kwenye kipindi cha mafundisho ya waongofu wapya tena alikuja tu kusalimia. Natamani ufahamu kuwa maombi yako sio bure wala machozi yako sio bure muujiza wako uko njiani unakuja japo hatujui ni wapi utatokea na sa ngapi na kwa namna ipi maadamu tu iwe ni kwa utukufu wa Bwana,sasa wapo watu leo ambao wameachishwa kazi kwa hila na hali familia nzima ilikuwa inawategemea kwa hiyo kazi ,wengine wameshitakiwa kwa uongo mpaka wakawekwa magerezani, wapo wanawake ambao baada ya waume zao kufariki wakapokonywa mali zote wamebaki na uchungu moyoni na wana watoto, ni muhimu kufahamu hili siku zote kuwa Mungu amehaidi kuto kukuacha wala kukupungukia endapo utaamua kumuamini na kumtegemea, ukisoma katika Zaburi 37:5 anasema "mkabidhi Bwana njia yako,pia umtumaini nae atafanya" hivyo basi hata kama jambo limekukatisha tamaa vipi usiache kumkabidhi Bwana na si tu kumkabidhi bali pia kuamini kuwa ulicho muomba atafanya ukisoma ule mstari wa 25 utakuta anasema "Nalikuwa kijana nami sasa ni mzee,lakini sijamwona mwenye haki ameachwa,wala mzao wake akiomba chakula,"watu wengi huwa hawajui namna Mungu anavyowathamini na kuwaheshimu hata kama wanapita katika magumu Daudi alipoifahamu siri hii ya ajabu akasema hajaona mwenye haki ameachwa maana yake ni kuwa hata kama ilitaka kuonekana kama ameachwa lakini baadae ikagundulika kumbe Mungu alikuwa amemkusudia jambo,ukishalifahamu hili kule kuamini tu kuwa Mungu atakupigania au Mungu amehaidi kunitetea huwa kunavuta msaada wa Mungu wa kukusaidia na kukuondolea hali ya hofu na mashaka na kukufanya uishi kwa imani na ujasiri.zaidi.
Wapo watu ambao wameachwa na wake zao au waume zao, na wameachiwa watoto na baadae kusikia yule mwanamke au mwanaume anataka kuolewa au kuoa kwingine , maumivu haya huwa yanakuwa ni mabaya sana tena mara nyingi yenye kuambatana na uchungu mkubwa maana si kitu kinachoelezeka kiurahisi hata kidogo, nakumbuka nilipata kumsikia mama ambae baada ya kuolewa na kuzaa watoto kadhaa ile mimba iliyofuata Mme wake akaikataa na kusema hiyo si yake na kuwa huyu mama amezini nje na hivyo basi ameamua kwenda kuoa mke mwingine maana ile haikuwa mimba yake, ni kitu kigumu sana na pia hakielezeki kirahisi sasa huyu mama ameachwa ni mjamzito,alafu amesingiziwa kazini nje,alafu anaambiwa mme wake anataka kuoa amepata na mchumba wa kumuoa, ni lazima tu maumivu yatakuwa ni makali sana moyoni, lakini kumbuka Biblia imeshasema katika Mithali 23:18 kuwa "Maana bila shaka iko thawabu,na tumaini lako halitabatilika." Kibinadamu huwezi kuelewa mambo Fulani yanapo kufika, lakini Biblia ni amina na kweli ikiwa unamuamini Mungu hakuna gumu kwa Mungu na tumaini la mwenye haki haliwezi batilika
BIBLIA INASEMA NINI JUU YA MAJARIBU NA MAGUMU UNAYOKUTANA NAYO
Ni wazi kabisa kuwa watu wengi wanakutana na hali za kuvunja moyo,wengine wamekatishwa tamaa kabisa,na wengine, ni vile tu yale waliyo yategemea yangetokea hayakutokea ,lakini nataka ujue ya kuwa Yesu yu hai leo maana kama asingalifufuka imani yetu ingekuwa ni bule,lakini maadamu alifufuka basi liko tumaini, hivyo basi endelea kuliamini neno lake na kumtumaini Yeye peke yake ukisoma Ufunuo 3:10anasema "kwa kuwa umelishika neno la subira yangu,mimi nami nitakulinda utoke katika saa ya kujaribiwa,,,,,,,,,,,"Maana ya kulishika neno la subira ni kule kuishi katika hali ya kumtumaini Mungu na kuliamini Neno lake {kule kujua neno lake li hai tena lina nguvu,kule kujua kuwa analiangalia hilo neno lake apate kulitimiza, hata kama halijatimizwa kwako bado, maana .inawezekana mazingira yanayo kuzunguka yakawa yanakukatisha tamaa kabisa hivyo basi ile tu kuwa na tumaini kwa Bwana kwa wakati kama huu, kutakufanyia mlango wa wewe kuweza kutoka, sasa ukulifuatilia lile neno "kwa kuwa umelishika neno la subira yangu"tunaweza tukatafsiri kama kwa sababu umelishika neno la subira yangu, hii ina maana kuwa kule kulishika neno la subira yake katika wakati kama huu wa magumu na mambo ya kukatisha tamaa ndiko kunakomfanya yeye akulinde na akusaidie kutoka kwenye wakati mgumu ulio nao,ikiwa ni pamoja na shida zinazo kuzunguka,

ukisoma huu mstari utaelewa vizuri kitu ninachotaka ukipate "Rumi 4:18:-21 Naye aliamini yasiyoweza kutarajiwa ili apate kuwa Baba wa mataifa mengi, ninachotaka ujue ni kuwa suara la Ibrahimu kuwa Baba wa mataifa mengi lilitegemea kule kumuamini Mungu na kulishika neno la subira yake hata kama kibinadamu mambo yalikuwa yanakatisha tama, ili kujua yalikuwa yanakatisha tamaa kivipi ukiendelea mbele kidogo utaona Biblia inasema aliamini yasiyoweza kutarajiwa maana yake ni kuwa aliamini vitu ambavyo hakuna mtu mwenye akili timamu asiyemuamini Mungu angeweza kukubaliana navyo, mstari wa 19 anasema "Yeye asiyekuwa dhaifu wa imani alifikiri hali ya mwili wake uliokuwa umekwisha kufa akiwa amekwisha kupata umri wa kama miaka mia na hali ya kufa tumbo lake sara."Mstari huu unaelezea jinsi ambavyo Ibrahimu alikuwa amezeeka vya kutosha na jinsi ambavyo Sara hata tumbo lake tu lilikuwa limekufa maana yake hawezi tena kupata mtoto kwa namna ya taratibu za kibinadamu, na bado Mungu aliendelea kuwahaidi hata katika wakati huu, kwao lilikuwa ni jaribu zito na hali iliyowakatisha tamaa kabisa kwa sababu walikuwa na mali nyingi ila hazina mrithi,na bado hawaoni kama kuna kitu kinaweza kikafanyika. Nini kiliwasaidia katika wakati kama huu ukisoma ule mstari wa 20 na 21 utakuta anasema "Lakini akiiona ahadi ya Mungu akusita kwa kutokuamini bali alitiwa moyo kwa imani akimtukuza Mungu huku akijua hakika ya kuwa Mungu aweza kufanya yale aliyoahidi kama kilichomsaidia Ibrahimu ni kutosita, kwa tafsiri nyingine ni kutokuwa na mashaka na huku hakujua hakika kuwa Mungu anaweza kufanya yale aliyohaidi,ndugu yangu unayesoma mafundisho haya bila kujalisha unapita katika kipindi cha namna gani liamini neno la Mungu amini ahadi za mungu juu ya maisha yako, Ibrahimu alimtukuza Mungu huku akijua hakika kuwa anaweza kufanya yale aliyohaidi.
NAMNA YA KUITAMBUA MILANGO YA KUTOKEA UWAPO KATIKATI YA MAJARIBU.
Ukisoma katika 1korinto 10:13 anasema, "Jaribu halikuwapata ninyi, isipokuwa lililo kawaida ya wanadamu;ila Mungu ni mwaminifu; ambae hatawaacha mjaribiwe kuliko mwezavyo lakini pamoja na lile jaribu atafanya na mlango wa kutokea,ili muweze kustahimili" anaposema jaribu halikuwapata ninyi isipokuwa lililo kawaida ya mwanadamu hii ina maana haijalishi tatizo unalokutana nalo limebeba vitisho vya namna gani,au watu wanasema kwa namna gani, au limekuumiza kwa kiwango kipi, cha msingi tu limekupata wewe basi hilo ni lakiwango chako, ndio hasa maana ya huu mstari unaosema jaribu halikuwapata ninyi isipokuwa lililo kawaida ya mwanadamu, hivyo basi hakuna jaribu linalo ruhusiwa kwako kinyume cha imani yako, na ndio sababu Yesu alipokuwa akiwafundisha wanafunzi wake kusali kipengele kimojawapo kilikuwa ni kumuomba Mungu asitutie majaribuni na kama kipengere hiki kilikuwa ni sehemu ya sala,hii ina maana majaribu sio mazuri, sasa basi mpaka jaribu likatokea kwako au likaruhusiwa kwako hii ni lazima kunasababu.hivyo basi kaa mkao wa kuona Mungu akikushindia na tamani kuona matokeo ya ushindi wako. Na majaribu siku zote ni sawa na mtihani na lengo la mtiani ni kukuvusha darasa hivyo basi jaribu lengo lake ni kukutoa kwenye kiwango Fulani cha imani na kukupeleka kwenye kiwango kingine, na ndio sababu Biblia ikasema tunatoka tunatoka utakatifu hadi utakatifu, pia tunatoka imani hadi imani na pia ni muhimu ukafahamu kuwa lengo la jaribu sio kukuangusha wewe,wala sio kukukatisha tamaa isipokuwa ni kuimalisha imani yako utakapokuwa umeshinda, hebu kwanza tuangalie huu mstari vizuri, anaposema "Lakini pamoja na lile jaribu atafanya na mlango wa kutokea ili muweze kustaimili" ninachotaka uone hapa ni kuwa pamoja na kwamba kila jaribu litakalo kuja kwako ni la kiwango chako bado Mungu amehaidi kufanya mlango kwa ajili ya wewe kustaimiliSasa ikiwa Mungu alihaidi kufanya mlango ili watu waweze kustaimili na bado watu wameanguka kwenye majaribu, hii haina maana majaribu yalikuwa mazito sana isipokuwa watu hawakuitambua milango ya kutokea maana yeye si mwongo alishasema atafanya mlango wa kutokea ili waweze kustaimili sasa kama amefanya mlango na mtu hakutoka basi inawezekana mtu hajatambua mlango au hakuchukua hatua ya kutoka.

Nini maana ya kutokuitambua milango ya kutokea
Wapo watu ambao katikati ya mapito na mambo magumu anayo kutana nayo anajisemea maneno ya laana, anaruhusu hali ya uchungu moyoni na si kwamba hajui anachokifanya ila ameamua tu kufanya hivyo {mara nyingi mwisho wake huwa unakuwa ni kuanguka} kwa sababu unaporuhusu maneno ya kukuvunja moyo tena unayo jitamkia mwenyewe kuna kitu kibaya kinachoumbika katika ulimwengu wa Roho {Mith 10:11}anasema "kinywa chake mwenye haki ni chemchem ya uzima bari jeuri hufunika kinywa chake mtu mpumbavu" sasa neno la Mungu limesema kinywa chako wewe mwenye haki bila kujalisha uko kwenye kipindi gani kinajulikana kama chenye chemchemu ya uzima, na sio laana japo kinao uwezo wa kutengeneza laana,Huu si wakati wa kujisemea mabaya ni wakati wa kusema najua bwana atanisaidia,najua ni kwa muda tu,Mungu ataniinua, Muujiza wangu unakuja,Bwana atafanya njia hiki ni kipindi cha kujitia Moyo Mwenyewe na usisubiri mtu mwingine,maana anaweza asitokee, maana haya maneno unayojitamkia yananafasi ya kujenga kitu au kubomoa kitu katika ulimwengu wa Roho Mithali 12:14 "Mtu atashiba mema kwa matunda ya kinywa chake na atarudishiwa matendo ya mikono yake" ikiwa hivyo ndivyo ilivyo kuwa muangalifu sana maana maneno yako na mawazo yako vinanafasi kubwa sana ya kuondoa uchungu uliotokea ndani yako. Maana kule kuendelea kuruhusu hali ya uchungu kutakuletea kukata tamaa na hatimae kumuacha Yesu na kuanguka dhambini.

MAMBO YA KUZINGATIA UWAPO KATIKATI YA MAJARIBU NA MAMBO MAGUMU
Huu si wakati wa kukaa na watu wanao kuvunja moyo na kukupandikiza roho za uasi ikiwa ni pamoja na kukata tamaa, wakikunenea maneno magumu maana wapo watu wanao ruhusu mazingira ya namna hii hata ikiwa wamejua madhara yake. {Na mara nyingi mwisho wake huwa unakuwa ni kurudi nyuma au kuanguka}ukisoma katika Mithali 12:5-6 anasema "mawazo ya mwenye haki ni adili,bali mashauri ya mtu mwovu ni hadaa", hivyo basi hiki ni kipindi cha kuwa muangalifu sana na watu wanao kushauri, sasa ukiendelea ule mstari wa sita utakuta anasema "Maneno ya waovu huotea damu,bali kinywa cha wanyofu kitawaokoa" anaposema kinywa cha wanyofu kitawaokoa hii ina maana kuwa unahitaji watu ambao ndani yao hamna hila, ili kukutia moyo maana pia ndani yao huwa kunakuwa na matumaini, na hivyo basi imani yako juu ya msaada wa Mungu kukusaidia inakuwa kubwa kabisa bila kujalisha ni magumu ya aina gani uanayo kutana nayo .
Huu si wakati wa kuwaza kulipiza kiasasi juu ya mtu aliye kutendea ubaya maana kuna watu huwa wanapita katika kipindi Fulani cha ugumu tu kwa sababu kuna mtu amemfanyia ubaya, pamoja na hayo kumbuka huu ni wakati wa kujitahidi kusamaehe,kuachilia nafsi yako maana kisasi ni juu ya Bwana ukisoma katika 2timotheo utaona Paulo akimwambia Thimotheo jinsi amabavyo Iskanda alimfanya apite katika kipindi kigumu sana maana alikuwa akimpinga sasa ukiendelea anaishia kusema Bwana atamlipa, maana anajua hatakiwi kulipiza kisasi 2Timotheo 4:14 anasema "Iskanda mfua shaba,alionyesha ubaya mwingi kwangu Bwana atamlipa sawasawa na matendo yake nawe ujihadhari na huyo,kwa sababu aliyapinga sana maneno yetu".
Huu si wakati wakumuelezea kila mtu yaliyotokea kwenye maisha yako, maana kuna wakati mwingine atavunjwa moyo kabisa na mtu uliyetegemea labda ndie angekutia Moyo pia hata kukusaidia kwa maombi kwa wakati kama huu, hivyo basi muombe Mungu akusaidie kujua ni yupi hasa atakuwa tayari kuubeba mzigo wako kwa wakati kama huu, ukisoma katika Isaya 35:3 utakuta anasema "Itieni nguvu mikono iliyo dhaifu,yafanyeni imara magoti yaliyolegea,Waambieni walio na hofu, "jipeni moyo msiogope? Unahitaji watu wa namna hii hasa upitapo katika magumu watakao kusaidia kuvuka, watakao kuambia jipe moyo na hatimae kutoka salama.
Huu si wakati wa kupokea kila ushauri maana unapokuwa unapita katika gumu Fulani ni rahisi sana kutaka kulitendea kazi kila unalolisikia,maana unafikiri ndani ya kila unalolisikia kuna uponyaji unaweza kupatikana, na wengine kipindi kama hiki huwa tayari kuombewa kila mahali au popote hata akiambiwa kuna mganga anaombea watu kwa kuagua yuko tayari kwenda bila kuhoji, kumbuka magumu ni kwa kitambo kifupi tu yasikufanye ukaharibu maisha yako na kumkosea Mungu kabisa, ukisoma Zab 23:4 anasema ,"nijapopita kati ya bonde la uvuli wa mauti sintaogopa mabaya;kwa maana wewe upo pamoja nami gongo lako na fimbo yako vyanifariji." Ni muhimu ukafahamu kuwa mfalme Daudi ni mmoja wa watumishi wa Mungu waliopitia kipindi kigumu sasa aliposema nijapopita alikuwa anamaana ya kujitia moyo kuwa sintakaa kwenye haya magumu siku zote isipokuwa ninapita tu,ndio maana akasema nijapopita sio nijapokaa,amini tu kuwa unapita,na ni kwa muda tu,
Huu si wakati wa kutumia muda mwingi sana kukifikiria kilicho tokea na jinsi kilivyo kuumiza maana utaishia tu kuwa na uchungu moyoni hata kupata vidonda vya tumbo na hata kumkosea Mungu, ipo mithali inasema yaliyopita si ndwele tugange yajayo,inawezekana yaliyotokea yamekuhaibisha,yamekutia aibu,yamekushusha hadhi, yamekuondolea heshima kwenye familia au jamii inayokuzunguka, bila kujalisha ilitokeaje cha msingi yameshatokea, wewe msii tu Mungu afanye kitu kipya kwako na si kulia tu huku ukiwa kwenye mawazo muda wote.baada ya Paulo kuamua kuyasahau yaliyo pita,kujikubali nafsi maana aliyafanya mambo mengi ya aibu kabla ya kumjua kristo,pale tu alipoamua kuutafuta uso wa Mungu kwa bidii baada ya kuamua kuyasahau yaliyo pita, Mungu alikuwa akijidhiirisha kwake siku hadi siku. Ukisoma Filipi 3:13 anasema Ndugu,sijidhanii nafsi yangu kwamba nimekwisha kushika;ila natenda neno moja tu;nikisahau yaliyo nyuma,nikiyachuchumilia yaliyo mbele nakaza mwendo,niifikilie mbele ya thawabu ya mwito mkuu wa Mungu katika kristo Yesu." Sasa basi kule kujitahidi kuyasahau yaliyopita kutakusaidia kukaza Mwendo na kujipanga upya kwa ajili ya yale yaliyo mbele yako.
Huu si wakati wa kuanza kujaribisha imani zingine, kama hujawahi tumia Dawa za kienyeji kwa sababu unaamini ni machukizo mbele za Bwana au kutambika kwa kutoa sadaka kwenye makaburi ya mababu kwa nini ufanye hivyo tu kwa sababu ya gumu Fulani tena linalopita tu? Muamini Mungu maana yote yawezekana kwake yeye aaminie kumbuka "ukiwa muaminifu kwa madogo Mungu atakufanya kuwa muaminifu na kwa makubwa pia".
Huu ni wakati wa kukaa kwenye maombi, nakumbuka Bwana Yesu alikuwa ni muombaji lakini pia baada ya kutambua kuwa anakiendea kipindi kigumu, muda mwingi aliendelea kukaa kwenye maombi zaidi na Mungu alikuwa akimtia nguvu ukisoma "Luka 22:40 anasema, "Alipofika mahali pale akawaambia "Ombeni kwamba msiingie majaribuni." Mwenyewe akajitenga nao kiasi cha kutupa jiwe,akapiga magoti akaomba akasema "Ee Baba, ikiwa ni mapenzi yako,uniondolee kikombe hiki;walakini si mapenzi yangu bali yako yatendeke." ninachotakaka uone ni kuwa alikuwa anapita katika jambo gumu sana tena la mauti ya msalaba hivyo alifika mahali pa kujihurumia nafsi yake, lakini kule kukaa kwenye maombi kwa wakati kama huu kulikuwa ni kwa muhimu sana ukisoma ule mstari wa 43 anasema "Malaika toka mbinguni akamtokea akamtia nguvu" hivyo tunaona malaika wa Bwana alimkuta Yesu kwenye maombi, pia kwa wasomaji wa biblia utakumbuka siku nyingine walikuja Musa na Elia lengo lilikuwa ni moja tu kumtia moyo BwanaYesu lakini walimkuta akiwa kwenye maombi,hivyo basi maombi huuisha, hitia nguvu, pia humtengenezea Mungu mazingira ya kujifunua kwako hata katika hilo unalolipitia wewe.
Huu si wakati wa kujilaani, kujikataa, na hata kufikiria ni bora ungekufa, ni muhimu kufahamu kuwa wewe ni wathamani sana mbele za Mungu bila kujalisha nini kimetokea kwenye maisha yako,anza kujinenea maneno yenye baraka,ushindi,mafanikio,uzima,huku ukimuamini Mungu.
Huu ni wakati wa kutafuta kujua ni mianya ipi ambayo ilimpa Adui nafasi kwenye maisha yako, na kujitahidi kutokumpa tena nafasi kwenye maisha yako huku ukilisoma neno la Mungu, na kukaa kwenye maombi ukijiepusha kabisa na mazingira yoyote yanayoweza kusababisha maumivu na uchungu moyoni.
Huu ni wakati wa kujifunza kujisamehe, Pamoja na kukubaliana na hali iliyotokea kuwa imeishatokea, kwa lengo la kuweka mikakati mipya ya maisha na si kuishia kujilaumu na kulia tu, kitu ambacho hakisaidii isipokuwa kuendelea kukutengenezea uchungu na majeraha moyoni.
Huu ni wakati wa kubadilisha mfumo wa mawazo usiendelee kukubaliana na mawazo ya kukukatisha tamaa wala kurudisha nyuma pia yale yanayokutaka ufanye kosa la pili maana wapo mabinti ambao baada ya kugundulika ana Mimba huamua kuitoa,kumbuka ni machukizo kwa Bwana maana wapo watu wanaomtafuta huyo mtoto usiku na mchana kubaliana na hali iliyotokea Rudi mbele za Mungu kwa toba, kasha anza kufikiri kwa habari ya maisha mapya na umuombe mungu akusaidie bila kujalisha jamii inakuchukuliaje maana kama umefanya kosa la kwanza ukaamua kufanya na lile la pili ni muhimu kufahamu kuwa unachokipanda utakivuna.maana Mungu adhihakiwi.
Huu ni wakati wa kujifunza kutokana na yaliyotokea, huku ukifanya tathimini kujua nini lilikuwa tatizo,au chanzo cha hilo jambo kilikuwa ni kitu gani, nani alihusika zaidi, na je yaliyofanyika yalikuwa ni mapenzi ya Mungu au la, ni Ni nini hasa neno la Mungu linasema kuhusu hilo jambo,ukishapata nafasi ya kutathmini kilichotokea ndipo sasa unaweza ukapata kitu cha kujifunza, au kuomba toba Mbele za Mungu na kufanya maamuzi yenye busara
Huu ni wakati wa kuijenga nafsi yako kwa neno la Mungu anza kujitahidi kujaza Moyo
wako neno la Mungu, Bwana Yesu siku moja alitoa sababu ya watu kupotea au kukosea kuwa ni kwa kutokulijua neno la Mungu, na hauwezi kulijua neno la mungu ikiwa haulisomi Mathayo 22:29 inasema "Yesu akajibu akawaambia "mwapotea"kwa kuwa hamyajui maandiko wala uweza wa Mungu" sasa ukisoma ile tafsiri ya kiingereza utakuta anasema your mistaken not knowing the scriptures tafsili ya moja kwa moja ya Kiswahili ni kuwa mnafanya makosa kwa sababu ya kutojua maandiko pia neno la Mungu limesisitizwa kujaa kwa wingi ndani yako kule kuendelea kulishika neno la Mungu na kulijaza kwenye nafsi yako ni kwa muhimu sana hasa kwa wakati kama huu.





MAMBO YA KUZINGATIA UNAPOKUWA UMEZUNGUKWA NA MAMBO YA KUKATISHA TAMAA
Endelea kumuamini, kumtii na kumtegemea Mungu peke yake hata uwapo katika hali ya kukatisha tamaa. Mke wa ayubu aliona ni bora Ayubu akufuru afe ili yale mateso yaishe,hii ina maana Ayubu alikuwa katika hali ya kukatisha tamaa kabisa, lakini bado aliendelea kumtegemea na kumtumaini Mungu peke yake pia ukisoma Luka 18:7anasema "na Mungu, je, hatawapatia haki wateule wake wanao mlilia mchana na usiku,nae ni mvumilivu kwao,nawaambia atawapatia haki upesi;" amini maombi yako na machozi yako mbele za Mungu sio bure na kuwa Mungu amehaidi kukupatia haki upesi endapo utamtumaini na kumtegemea yeye peke yakeJapo pia inawezekana ukawa umetishiwa mambo mabaya, wanataka kukudhulmu,kukuua, unakaliwa vikao vya hila, neno linasema katika Zaburi 125 :2 "kama milima inavyozunguka yerusalemu,ndivyo bwana anavyozunguka watu wake,tangu sasa na hata milele" ukiufuatilia ule mstari wa 3a utakuta anasema "kwa maana fimbo ya udhalimu haita kaa juu ya fungu la mwenye haki" na endapo wakawa wamekudhurumu mali umesingiziwa, mambo ambayo hujayafanya Biblia inasema Math 5:11 "Heri ninyi watakapowashutumu na kuwaudhi na kuwanenea kila neno baya kwa uongo,kwa ajili yangu. Furahini, na kushangilia,kwa kuwa thawabu yenu ni kubwa mbinguni hii isiwe kwa ajili ya kukuvunja moyo bali iwe ni gia ya kukufanya usonge mbele.
Usiache kukaa kwenye maombi uwapo katika wakati huu Biblia inasema katika "Filipi 4:6 Msijisumbue kwa neno lolote bali katika kila neno kwa kusali na kuomba,pamoja na kushukuru,haja zenu na zijulikane na Mungu"hiki ni kipindi cha kukaa kwenye uwepo wa Mungu sana maana wengi walimuacha Yesu tu kwa sababu ya uchungu na Magumu waliyowahi kukutana nayo kumbuka hujaanza wewe wengi walipita katika hayo na Mungu akawashindia..Neno la Mungu linasema katika Math 7:7 "Ombeni nanyi mtapewa;tafuteni nanyi mtaona; bisheni nanyi mtafunguliwa; kwa maana kila aombae hupokea naye atafutae huona;nae abishae atafunguliwa" ndugu msomaji endelea kuomba bila kuchoka maana neno la Mungu linasema kila aombae hupokea amini ipo siku utapokea muujiza wako, tena Bwana Yesu akitaka kusisitiza kuhusika kwake katika mambo yako akasema kwenye ule mstari wa 9 Au kuna mtu yupi kwenu, ambae mwanawe akimuomba mkate atampa jiwe au akimuomba samaki atampa nyoka? Basi ikiwa ninyi mlio waovu,mnajua kuwapa watoto wenu vipawa vyema,je si zaidi sana Baba yenu aliye mbinguni atawapa mema wao wamuombao" Lakini pia BwanaYesu akijua kuna watu watakata tamaa kabla ya kupokea miujiza yao akawaambia mfano ukisoma Luka 18:1 anasema "Akawaambia mfano ya kwamba imewapasa kumuomba Mungu siku zote,wala msikate tamaa Yesu alijua kuna watu watakata tamaa upesi ikabidi atoe na mifano mstari wa 2 akaendelea kusema "palikwa na kadhi katika mji Fulani,hamchi Mungu, wala hajali watu na katika mji huo palikuwa na mwanamke mjane,aliyekuwa akimuendea endea,akisema,nipatie haki na adui wangu nae kwa muda alikataa;alafu akasema moyoni mwake,Ijapokuwa simchi Mungu wala sijali watu lakini kwa kuwa mjane huyu ananiudhi nitampatia haki yake asije akanichosha kwa kunijia daima."’sasa ukiendele mstari wa sita unaona msisitizo wa jambo baada ya mfano "Bwana akasema, Sikilizeni asemavyo yule kadhi dhalimu.Na Mungu je hatawapatia haki yake wateule wake wanao mlilia mchana na usiku,naye ni mvumilivu kwao nawaambia atawapatia haki upesi kwa tafsiri nyingine ni kuwa kama tu yule kadhi asiejali mtu wala Mungu bado alifika mahali akaona huyu Mama anamsumbua kiasi ambacho ni bora tu ampatie hitaji lake Si zaidi Mungu wa mbinguni na wewe ukiwa kama mtoto wake. Muamini Mungu usikate tamaa atakupatia haki yako upesi.
Jifunze kumtwika yesu fadhaa zako hii ndio ilikuwa sababu ya yeye kufa msalabani, kumbuka alipokuwa pale msalabani alisema imekwisha ukisoma Isaya 53:4a anasema "Hakika ameyachukuwa masikitiko yetu,amejitwika huzuni zetu" hivyo basi hayo masikitiko yako, hizo huzuni zako Yesu alivichukuwa msalabani, ukisoma ule mstari wa 5 anasema "bali alijeruhiwa kwa makosa yetu,alichubuliwa kwa maovu yetu.Adhabu ya amani yetu ilikuwa juu yake na kwa kupigwa kwake sisi tumepona."ukisha kuyaona hayo muamini Mungu Lakini pia ukisoma 1petro 5:7 anasema "huku mkimtwika yeye fadhaa zenu zote maana yeye hujishugulisha sana na mambo yenu" maana ya kumtwika yeye fadhaa zako ni kumbebesha mzigo wako,na sio kubaki na mzigo wako Amini Mungu anajishugulisha sana na mambo yako na amini yuko tayari kubeba mateso yako hata kama mazingira yanaonyesha ugumu wa kila namna.
Amini tu kuwa Mungu atatenda Biblia inasema nini juu ya kuamini ukisoma Ebrania 11:6 anasema Basi imani ni kuwa na hakika juu ya mambo yatarajiwayo,ni bayana ya mambo yasiyoonekana. Kama imani ni kuwa na uhakika juu ya mambo yatarajiwayo hii inamaana hayapo, wala hayaonekani, ila unayategemea, na anaposema ni bayana ya mambo yasiyoonekana maana yake, ni ukweli juu ya kitu ambacho hakipo wala hakionekani kwa macho pia kinaweza kisiwe hata na dalili zozote kuwa kinaweza kutokea ila wewe unakiona bayana kwa kutarajia ukiamini,ndio sababu ukisoma Rumi 4:18a anasema "Naye aliamini kwa kutarajia yasiyoweza kutarajiwa" hii Ina maana kuwa, aliyaona bayana mambo ambayo hakuna mtu aliyategemea yangetokea ila yeye aliendelea kuamini huku akiyategemea yatokee anaposema aliamini kwa kutarajia maana yake aliamini kwa kusubiria
Kaa mkao wa kuepuka mabaya huku ukitarajia muujiza wako toka kwa BwanaJambo linalo sababisha watu wengi leo wasipokee miujiza yao kutoka kwa Mungu ni kutokaa mkao wa kutarajia toka kwa Bwana hata kama wamekuwa wakiomba,wengi mnafahamu mnapokua mkimtarajia mgeni Fulani nyumbani kila hodi inayogongwa huwa mnafikilia ni yeye, kwa nini? kwa sababu mnamtarajia mgeni, hebu fikiria huu mfano wa kawaida ndio Askofu wako amesema anakuja nyumbani kwako, jinsi unavyo jiandaa kuweka kila kitu safi tena kila kitu mahali pake,na hata kama kuna ratiba huwa zinaendelea hapo nyumbani siku hiyo inakuwa tofauti kwa nini kwa sababu tu unatarajia mgeni, mfano wa pili ni mama mjamzito anapotarajia kujifungua kuna baadhi ya vitu huwa anakuwa hawezi kufanya kwa sababu anajua akifanya vinaweza kuharibu tarajio lake alilo nalo juu ya ujio wa kiumbe kipya.hivyo basi kaa mkao wa kuona Mungu akikutetea acha kujilaani, na kujikatia tamaa, anza kujiamini huku ukitarajia muujiza wako toka kwa bwana.Sasa basi unapokuwa umepita kwenye magumu huu sio wakati wa kujichafua isipokuwa kujitakasa na kutegemea kumuona Mungu akikusaidia,maana kule kujichafua na kuanza kufanya mambo yasiyompendeza Mungu ndiko kunakoweza kusababisha usipokee muujiza wako toka kwa Mungu, naamini kabisa kuwa mpaka sasa Mungu ameshafanya kitu kukubwa kwenye maisha yako kupitia somo hili, endelea kumuamini na kumtegemea Bwana Yesu siku zote za maisha yako. Mungu na akubariki sana. USIACHE KUTUOMBEA.
Mwl: Tuntufye Andew mwakyembe
Email tumsifu_Andrew@yahoo.com simu 0784 629562 na kwa uhitaji wa maombezi youth_ prayernet@yahoo.com pia C/o S.L.P 55 USA RIVER ARUSHA
ENDAPO UMEGUSWA NA HUDUMA HII NA UNGEPENDA KUPANDA MBEGU KWA KUSAIDIA KULIPIA SEHEMU YA GHARAMA
usisite kuwasiliana nasi.au waweza kutumia account No.016201033820 NBC.MBEYA BRANCH.
Kwa maelezo zaidi tumia Email ifuatayo yagotm28@yahoo.com